Mtoto wako anahitaji kutumia dawa inayoitwa hydroxyurea. Karatasi hii ya maelezo inaeleza jinsi hydroxyurea inavyofanya kazi na jinsi inavyotolewa kwa mtoto wako. Pia inaeleza madhara au matatizo ambayo mtoto wako anaweza kupata anapotumia dawa hii.
Hydroxyurea ni nini?
Hydroxyurea ni dawa ya tibakemikali ambayo imetumika kutibu magonjwa mengi, ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa selimundu. Utafiti umeonyesha kuwa wagonjwa wa selimundu wanaochukua hydroxyurea:
- wanalazwa hospitalini kwa sababu ya matukio ya maumivu mara nusu ya mara ambazo wagonjwa ambao hawachukui hydroxyurea
- wana visa vichache vya ugonjwa mkali wa kifua.
- wanahitaji upaji kiasi wa damu ikiwa wanalazwa hospitalini
Unaweza kusikia hydroxyurea ikitajwa kwa jina lake la chapa, Hydrea. Hydroxyurea inapatikana katika umbo la kidonge.
Mtoto wako anaweza kupatiwa hydroxyurea ikiwa
- wamelazwa mara tatu au zaidi hospitalini kwa matukio makubwa ya maumivu katika miezi 12 iliyopita
- wamehitaji upaji wa damu mara moja au zaidi kwa ajili ya kisa kimoja au zaidi cha ugonjwa mkali wa kifua
- wamepoteza muda mkubwa kutoka shuleni au kazini kutokana na matukio ya maumivu ambayo yameweza kudhibitiwa nyumbani
Kabla ya hydroxyurea kutolewa kwa mtoto wako
Mwambie daktari wa mtoto wako ikiwa mtoto wako amekuwa na majibu ya mzio kwa hydroxyurea au kiungo chochote cha muundo wake au ikiwa mtoto wako ana ugonjwa wowote wa kingamwili au damu (licha ya ugonjwa wa selimundu).
Zungumza na daktari au mtaalamu wa dawa wa mtoto wako ikiwa mtoto wako ana mojawapo ya hali zifuatazo. Tahadhari zinaweza kuchukuliwa na dawa hizi ikiwa mtoto wako:
- ana ugonjwa wa ini
- ana ugonjwa wa figo
- ana ujauzito
Hydroxyurea inatolewa vipi kwa mtoto wako?
- Mpe mtoto wako hydroxyurea kama daktari wako au mtaalamu wa dawa anavyokuambia. Zungumza na daktari wa mtoto wako kabla ya kusitisha kumpa dawa hii kwa sababu yoyote. Inaweza kuchukua miezi michache hadi athari zake kamili ziweze kuonekana.
- Upimaji wa damu unaweza kufanywa kila baada ya miezi miwili wakati wa kuanza dawa hii ili kupatikana dozi sahihi kwa mtoto wako.
- Mpe mtoto wako hydroxyurea mara moja kwa siku, karibu na wakati ule ule kila siku. Wagonjwa wengi hupendelea kuichukua wakati wa kulala.
- Unaweza kumpa mtoto wako hydroxyurea akiwa na chakula au bila chakula. Kumpa akiwa na chakula kunaweza kusaidia kuepuka maumivu ya tumbo.
- Mtoto wako anapaswa kunywa maji mengi (vinywaji) kila siku.
- Ikiwa mtoto wako atatapika chini ya nusu saa baada ya kuchukua hydroxyurea, mpe tena dozi ya dawa. Ikiwa mtoto wako atatapika zaidi ya nusu saa baada ya kuchukua hydroxyurea, usimpe tena dozi ya dawa. Mpe dozi inayofuata kesho kwa wakati wa kawaida.
- Hydroxyurea inatolewa kama kidonge cha 500 mg nchini Kanada. Mtoto wako anapaswa kumeza kidonge chote na glasi ya maji au kinywaji kingine.
- Ikiwa mtoto wako hawezi kumeza vidonge au anachukua dozi ndogo kuliko kidonge chote, angalia njia bora ya kumpa hydroxyurea na mtaalamu wa dawa. Kidonge kinaweza kufunguliwa na kuyeyushwa kwenye sindano ya dawa ili kumpa dozi iliyoamriwa. Tupa dawa iliyobaki.
- Mtaalamu wa dawa atakufundisha jinsi ya kushughulikia hydroxyurea kwa usalama, ikiwa ni pamoja na kutumia glovu unapochanganya poda kutoka kwa kidonge. Mtaalamu wa dawa pia atakufundisha jinsi ya kutupa dawa kwa usalama.
- Mtu yeyote anayeshughulikia hydroxyurea anapaswa kuosha mikono yao kabla na baada ya kugusa chupa au vidonge. Kwa maagizo ya kina kuhusu kushughulikia na kuhifadhi hydroxyurea kwa usalama, angalia. Tibakemikali nyumbani: Kumpa mtoto wako vidonge kwa usalama.
Unapaswa kufanya nini ikiwa mtoto wako anakosa dozi ya hydroxyurea?
- Ikiwa dozi imekosa, usimpe dozi ya ziada.
Inachukua muda gani kwa hydroxyurea kufanya kazi?
Inaweza kuchukua miezi michache kabla ya mabadiliko kuonekana katika vipimo vya damu.
Ni madhara gani yanayoweza kutokea kutokana na hydroxyurea na yanafuatiliwaje?
Mtoto wako anaweza kuwa na baadhi ya madhara haya wakati anapotumia hydroxyurea. Wasiliana na daktari wa mtoto wako ikiwa mtoto wako ataendelea kuwa na madhara haya na hayaponi, au kama yanamsumbua mtoto wako:
- Kichefuchefu na kutapika: Epuka kuchukua hydroxyurea ukiwa na tumbo tupu.
- Mapele ya ngozi: Haya yanaweza kuwa mapovu yasiyo maalum ambayo hupotea hata dawa ikiendelea kutumika. Ikiwa mapovu yatatokea, muone daktari aliyeandikia mtoto wako hydroxyurea.
- Kupoteza nywele: Kunaweza kutokea kupungua kwa nywele. Kupoteza nywele kawaida hakusababishi maeneo ya upara kwenye kichwa. Ikiwa hili litatokea, hatari na faida za kuchukua hydroxyurea (afya bora na matukio machache) inapaswa kujadiliwa na daktari wa mtoto wako ili kuamua kuhusu kuendelea na matumizi ya dawa hii.
- Kupungua kwa baadhi ya hesabu za damu: Mtoto wako anahitaji kupimwa damu ili kuangalia hesabu za damu kila baada ya miezi miwili kwa mwaka wa kwanza wa matibabu. Vipimo hivi vinaweza kufanywa katika maabara ya karibu na matokeo yatatumwa kwa daktari wa mtoto wako. Ikiwa hesabu zitakuwa chini ya kiwango kilichokubaliwa, utapigiwa simu kusitisha dawa na kurudia kupima damu baada ya siku saba. Hesabu kawaida hupona na dawa inaweza kuendelea kutumika kama ilivyoagizwa. Ikiwa hesabu za seli nyeupe zitapungua tena, basi dozi itapunguzwa hadi ile aliyokuwa akitumia mtoto wako kabla ya hesabu kuanza kupungua. Mtoto wako ataendelea kuchukua dozi hii ya chini.
- Ngozi na kucha kugeuka kuwa nyeusi: Baada ya kutumia hydroxyurea kwa muda, baadhi ya wagonjwa hupata weusi wa kucha na ngozi kwenye mikunjo kama vile kwenye viungo vya mikono. Athari hii hupotea mara tu dawa inapomaliza kutumika.
- Shida ya ini (matatizo): Hii ni nadra, lakini vipimo vya damu vinachukuliwa kila baada ya miezi mitatu ili kutathmini uwepo wa tatizo hili.
- Maumivu ya kichwa.
- Udhaifu wa misuli, hasa kwenye mapaja na mikono ya juu.
- Kuwashwa au vidonda kinywani: Kutumia brashi ya meno laini na kusafisha mdomo kunaweza kusaidia.
- Madhara ya muda mrefu: Hydroxyurea ni dawa ya tibakemikali, na baadhi ya dawa hizi zimehusishwa na wagonjwa kupata saratani baada ya miaka mingi. Lakini katika zaidi ya miaka 20 ya matumizi ya hydroxyurea kwa wagonjwa wa ugonjwa wa selimundu, hakujakuwa na ripoti yoyote ya dawa hii kusababisha saratani.
Ni hatua gani za usalama zinapaswa kuchukuliwa wakati mtoto wako anapotumia hydroxyurea?
Hydroxyurea inaweza kupunguza kwa muda hesabu za damu za mtoto wako, jambo linalomfanya kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi. Ili kuzuia maambukizi, mtoto wako anapaswa kuepuka watu wenye maambukizi, kama vile homa au mafua, hasa wakati hesabu za damu zao zikiwa chini.
Kuna hatari kwamba hydroxyurea inaweza kusababisha kasoro za uzazi ikiwa itachukuliwa wakati wa kushika mimba au ikiwa itachukuliwa wakati wa ujauzito. Ikiwa wewe ni msichana mdogo ambaye anajihusisha kimapenzi, unapaswa kutumia aina yoyote ya kinga ya uzazi wakati unapopokea hydroxyurea. Ikiwa utapata ujauzito wakati unachukua hydroxyurea, unapaswa kusitisha kuitumia mara moja na kumwambia daktari wako.
Unapaswa kusitisha kuchukua hydroxyurea kwa angalau miezi mitatu kabla ya kujaribu kupata ujauzito. Hydroxyurea pia inaweza kupunguza hesabu za mbegu za kiume.
Ikiwa mtoto wako ana Virusi Vya Ukimwi (VVU) na anachukua dawa kwa ajili ya hali hii, hasa didanosine na/au stavudine, zungumza na daktari wa mtoto wako.
Hii si orodha kamili. Wasiliana na daktari wa mtoto wako au mtaalamu wa dawa kabla ya kumpa mtoto wako dawa nyingine yoyote (za agizo, zisizo za agizo, za mitishamba, au bidhaa asili).
Kama mzazi au mlezi, hatari ya madhara kutokana na kushughulikia dawa hatarishi ni ndogo, hata hivyo, ni wazo zuri kupunguza au kuepuka kutangamana nayo. Hii inajumuisha kutoonja dawa ya mtoto wako. Pia, ikiwa wewe ni mjamzito au unanyonyesha, ni bora kuepuka kugusa dawa hatari. Ikiwa inawezekana, omba mtu mwingine ampe mtoto wako dawa.
Dawa hatari inaweza kuharibu seli zilizo na afya. Mtu yeyote anayeshughulikia dawa hatari anapaswa kujilinda. Unaweza kuvaa glovu na barakoa unaposugulikia dawa ya mtoto wako. Pia, kabla ya kuandaa dawa ya mtoto wako, osha mikono yako kwa sabuni na maji.
Ni taarifa nyingine zipi muhimu unapaswa kujua kuhusu hydroxyurea?
- Dawa hii inapaswa kuchukuliwa kila siku, siyo tu wakati shambulizi la maumivu linapoanza. Haitaondoa maumivu katika shambulizi linaloendelea. Inafanya kazi kwa kufanya mabadiliko kwenye seli za damu ambazo huzuia mashambulizi. Inapunguza kubadilika kwa seli, inapunguza kuharibika kwa seli nyekundu za damu, na kuongeza hemoglobini ya fetasi inayolinda.
- Katika ziara ya mwezi mmoja, seli nyekundu za damu ni kubwa. Hii inaonekana kupitia vipimo na kuangalia chini ya darubini. Seli hizi nyekundu za damu zina uwezo wa kupita kwa urahisi kupitia mishipa midogo ya damu na kuharibika kidogo. Wazazi mara nyingi wanasema kwamba hamu ya mtoto wao ya kula imeongezeka.
- Baada ya miezi mitatu ya kutumia dawa hii, pia kuna ongezeko la hemoglobini ya fetasi na kiwango cha jumla cha hemoglobini. Tunajua kwamba wagonjwa wenye viwango vya juu vya hemoglobini ya fetasi wana mashambulizi machache.
- Baada ya miezi sita, mtoto wako anapaswa kuwa na mashambulizi machache ya maumivu kuliko yale yaliyotokea miezi sita kabla ya kuanza matibabu.
- Muda ambao mgonjwa ataendelea kuchukua dawa hii utakuwa uamuzi kati yake na daktari anayemshughulikia.
- Hydroxyurea inajumuishwa katika mipango yote ya bima ya kibinafsi na mpango wa Faida za Dawa wa Ontario.
- Usiwape wengine dawa ya mtoto wako. Usimpe mtoto wako dawa ya mtu mwingine.
- Hakikisha kwamba daima unayo hydroxyurea ya kutosha ili ifikie mwisho wa wikendi, sikukuu, na likizo. Piga simu kwa famasia yako angalau siku mbili kabla ya mtoto wako kumaliza dawa ili kuagiza dawa mpya.
- Hifadhi hydroxyurea katika joto la chumbani mahali pa baridi na kavu, mbali na mwanga wa jua. USIhifadhi dawa hii bafuni au jikoni.
- Usihifadhi dawa yoyote ambayo imepitwa na muda wake. Angalia na mtaalamu wa dawa kuhusu njia bora ya kutupa dawa zilizopitwa na muda au zilizobaki.
Taarifa kuhusu kuzidisha dawa.
Hifadhi hydroxyurea mahali ambapo mtoto wako hawezi kuiona au kuifikia na ifungiwe mahali salama. Ikiwa mtoto wako atachukua kiasi kikubwa cha hydroxyurea, piga simu Kituo cha Mitaa cha Taarifa za Sumu kwa mojawapo ya nambari hizi. Simu hizi ni bure.
- Piga simu 1-844 POISON-X, au 1-844-764-7669, kutoka popote nchini Kanada isipokuwa Quebec.
- Piga simu 1-800-463-5060 ikiwa unaishi Quebec.
Kanusho: Taarifa katika Kijitabu hiki cha Msaada wa Dawa kwa Familia ni sahihi wakati wa kuchapishwa. Inatoa muhtasari wa taarifa kuhusu hydroxyurea na haitoi taarifa zote zinazowezekana kuhusu dawa hii. Si madhara yote yameorodheshwa. Ikiwa una maswali yoyote au unataka taarifa zaidi kuhusu hydroxyurea, zungumza na mtoa huduma yako ya afya.